Jaji Mkuu alaani utumiaji wa nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji

Martin Mwanje
2 Min Read

Jaji Mkuu Martha Koome amelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Polisi katika siku za hivi majuzi wameshutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano hayo katika hali inayodaiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa.

“Wakati katiba iliporuhusu kufanywa kwa maandamano ya amani bila silaha na kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka za umma katika kifungu cha 37, haikutazmaia yeyote kupoteza maisha yao wakati wakitekeleza haki yao,” amesema Jaji Koome leo Jumatatu asubuhi wakati alipoongoza hafla ya kula kiapo ya mawakili wapya 401 jijini Nairobi.

“Kwa hivyo, ninalaani matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ambayo tumeshuhudia na kutoa wito kwa wahusika kuadhibiwa na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria. Wajibu wa serikali ni kulinda maisha wala sio kuyaondoa.”

Kadhalika, Jaji Mkuu ametoa wito kwa wale wanaofanya maandamano kufanya hivyo kwa njia ya amani na katika njia ambayo si tishio kwa maisha au mali.

“Natoa wito kwa raia kutokiuka uaminifu ambao tumepewa na katiba katika kifungu cha 37 kwa kuharibu, kupora na kuteketeza mali ya umma na binafsi.”

Alisisitiza kuwa watu wote waliomakatwa wakati wa maandamano hayo ni sharti wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria na ndani ya muda ulioelezewa katika katiba.

Katiba inaelezea kuwa mtu yeyote aliyekamatwa anapaswa kufikishwa mahakamani katika muda usiozidi saa 24 baada ya kukamatwa.

 

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *