Mamlaka huru ya kutathmini utendakazi wa maafisa wa polisi nchini IPOA imeonya wananchi dhidi ya kushambulia maafisa wa polisi wanaotumwa nyanjani hasa wakati wa maandamano.
Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori amesema kupitia taarifa kwamba hatua hiyo inahujumu jukumu la polisi la kutoa ulinzi, inaondoa ulinzi wa wananchi kutoka kwa maafisa wa polisi kando na kudhihirisha kukosa kuzingatia sheria.
Katika taarifa hiyo ya leo Julai 3, 2024, Makori anaelezea kwamba wamefahamishwa kuhusu visa vya wananchi kushambulia kiyuo cha polisi cha Bondo katika kaunti ya Siaya ambapo maafisa waliokuwepo walishambuliwa.
Ametaja pia kisa cha afisa wa polisi anayehudumu katika kituo cha polisi cha Sigomere alishambuliwa na wananchi na kuachwa na majeraha makali.
Kulingana na Makori maafisa wa IPOA wamemzuru afisa huyo katika hospitali ya Maxcure mjini Kisumu ambapo anaendelea kupokea matibabu.
Makori alisema kama IPOA wataendelea kufuatilia kile alichokitaja kuwa mapungufu kwa upande wa maafisa wa polisi ambapo watapatikana wakitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wananchi.
Lakini alisema pia kwamba watafuatilia pia visa vya wananchi kushambulia maafisa wa polisi.