IGAD yatoa wito wa kusitishwa kwa vita Sudan

Tom Mathinji
2 Min Read

Shirika la IGAD limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu inayozorota nchini Sudan.

Dkt. Workneh Gebeyehu, ambaye ni katibu mtendaji wa IGAD kuhusu mchakato wa Jeddah, ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, kutoa fursa kwa misaada ya kibinadamu kutekelezwa.

Aliyasema hayo siku ya Jumanne katika ikulu ya Nairobi, katika mkutano na Rais William Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa IGAD kuhusu mzozo wa Sudan.

Dr. Wokneh alijukumiwa kuwakilisha IGAD katika mkutano wa Jeddah akiwa kiongozi mwenza pamoja na Saudi Arabia na Marekani, kujadiliana na wawakilishi wa Sudan Armed Forces (SAF) na Rapid Response Forces (RSF), ili kuafikia usitishwaji wa vita na kutoa fursa kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu.

Licha pande hizo mbili kukubaliana kuhusu utoaji wa misaada ya kibinadamu, Workneh alisema pande hizo bado hazijaafikiana kuhusu kukomeshwa kwa mapigano.

Huku akitaja hali hiyo kuwa ya dharura, katibu huyo alisema mashauriano yanaendelea miongoni mwa viongozi wa IGAD, kukubaliana kuhusu hatua itakayochukuliwa kusitisha mzozo huo.

Viongozi hao wawili walikutana siku moja baada ya Rais William Ruto kuwa mwenyeji wa kiongozi wa kijeshi wa Sudan Abdel-Fattah Al Burhan.

Ruto na Al Burhan walielezea haja ya kupatikana kwa suluhu kwa mzozo unaoghubika Sudan haraka iwezekanavyo.

Vile vile walikubaliana kuandaliwa kwa kongamano la mataifa ya IGAD, kwa lengo la kuharakisha mchakato wa Jeddah, ili kumaliza mgogoro unaoshuhudiwa Sudan.

Vita vilizuka mwezi Aprili, kati ya vikosi vinavyoongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na aliyekuwa naibu wake Mohamed Hamdan Daglo, anayeongoza vikosi vya dharura vya RSF.

Share This Article