IGAD yashinikiza juhudi za pamoja kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi

Tom Mathinji
2 Min Read
katibu mtendaji wa shirika la IGAD Workneh Gebeyehu,

Shirika la IGAD limesema kuna haja ya kuimarisha utabiri wa hali ya hewa pamoja na mifumo ya tahadhari ya mapema katika kanda hii.

Akizungumza siku ya Jumatatu wakati wa ufunguzi wa kongamano la 68 la mtazamo wa hali ya hewa wa upembe wa Afrika Jijini Nairobi, katibu wa shirika hilo Workneh Gebeyehu, alitoa wito wa umoja akielezea haja ya matumizi ya teknolojia ya kisasa, uvumbuzi na maarifa asilia ili kuwepo ustahimilivu miongoni mwa jamii utakaotumika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

Dakta Gebeyehu amesema katika kipindi cha siku mbili zifuatazo, wanaohudhuria kongamano, hilo wataangazia uimarishaji wa utabiri wa hali ya hewa pamoja na mifumo ya tahadhari ya mapema huku wakijumuisha habari kuhusu utabiri wa hali ya hewa katika sera za kitaifa na mipango ya maendeleo.

Gebeyehu alikariri haja ya juhudi za pamoja na kujitolea kwa shirika la IGAD kujenga ustahimilivu katika jamii ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Mabadiliko ya hali ya anga sio hatari iliyo mbali tena, lakini ni hatari inayokumba bara hili kwa sasa. Athari za mabadiliko ya Tabia Nchi kama vile ongezeko la viwango vya bahari na kupanda kwa nyuzijoto yanaathiri kote duniani,” alisema Dkt. Workneh.

Shirika la IGAD linasema linalenga si tu kuangazia changamoto za mabadiliko ya tabianchi bali pia suluhu na mapendekezo yatakayotoa mwongozo wa kipekee wa ustahimilivu na usalama kwa upembe wa Afrika.

Website |  + posts
Share This Article