Idara ya mahakama kuimarisha usalama wa majaji

Marion Bosire
2 Min Read

Idara ya mahakama imehaidi kuimarisha usalama wa majaji na maafisa wake wakiwa mahakamani.

Msajili Mkuu wa Idara hiyo Winfrida Mokaya ametoa hakikisho hilo Alhamisi kufuatia tukio kwenye mahakama ya Makarada saa nane alasiri ambapo hakimu Monica Kivuti alipigwa risasi na kujeruhiwa huku afisa wa polisi akiuawa.

“Tungependa kuwahakikishia maafisa wote wa mahakama, wafanyakazi na watumiaji wa mahakama usalama na usalama wao katika majengo yetu yote,” aliahidi Mokaya.

“Tutaimarisha itifaki zetu za usalama kwa raia wanaozuru mahakama zetu pamoja na maafisa wa usalama wanaotembelea mahakama katika hali ambazo hazihitaji kuwa na silaha.”aliongeza.

Hakimu huyo Mkuu alipigwa risasi muda mchache baada ya kutoa uamuzi kuhusu kesi dhidi ya mke wa afisa husika aliyeuawa katika tukio hilo.

Msajili huyo alizungumzia tukio hilo akishtumu mshtakiwa kwa kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kwa kukosa kuhudhuria kesi mahakamani baada ya kulipa dhamana.

“Wakati wa kikao cha wazi cha mahakama mapema leo, Hakimu alifuta dhamana kwa mshtakiwa ambaye alikosa kuhudhuria mahakama baada ya kulipa dhamana,” Mokaya alisema.

Mokaya alionyesha kusikitishwa kutokana na tukio hilo.

“Mara moja uamuzi huu ulipotolewa, mtu mmoja alimpiga risasi Hakimu na kumjeruhi kwenye nyonga,” alisema.

Alisema taarifa za awali zilieleza kuwa aliyempiga risasi ni askari polisi ambaye ni mumewe mshtakiwa.

“Tunamtakia mwenzetu afueni ya haraka. Pia tunatuma salamu za rambirambi kwa familia ya afisa huyo aliyepoteza maisha katika tukio hili la kusikitisha,” alisema.

Mokaya aliomba utulivu wakati uchunguzi ukiendelea kuhusiana na tukio hilo.

“Tunaomba utulivu kutoka kwa watumiaji wote wa mahakama kwani vyombo vyetu vya sheria vinachunguza zaidi tukio hili,” alisema msajili huyo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *