Idadi ya visa vya Mpox yagonga 31, Wakenya watakiwa kujihadhari

Martin Mwanje
1 Min Read

Wizara ya Afya imetoa wito kwa Wakenya kuchukua tahadhari zaidi huku idadi ya visa vya ugonjwa wa Mpox ikifikia 31 tangu kuanza kwa mlipuko wa ugonjwa huo nchini. 

Hii ni baada ya visa vipya 2 kuripotiwa katika kaunti za Nakuru na Mombasa, kisa kimoja katika kila kaunti.

“Wizara ya Afya imedhamiria kudhibiti mlipuko wa Mpox na kulinda afya na usalama wa Wakenya wote, hasa msimu huu wa sherehe,” amesema Waziri Deborah Barasa kwenye taarifa.

“Tunatambua juhudi zinazodhihirishwa na umma katika kutusaidia kudhibiti mlipuko huu na kuhakikisha usalama wa nchi yetu.”

Kulingana na Waziri Barasa, visa vya Mpox vimeripotiwa katika kaunti 12 kote nchini huku idadi kubwa ya visa ikiripotiwa katika kaunti ya Nakuru (10), Mombasa (8) na Nairobi (2).

Wasafiri zaidi ya milioni 2.6 wamepimwa katika maeneo mbalimbali ya kuingia nchini na visa vinavyoshukiwa kuwa vya ugonjwa huo kutambuliwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Wizara ya Afya inasema ili kukabiliana na mlipuko huo, inaendelea kushirikiana na serikali za kaunti na washikadau wengine kuhamasisha umma na kusisitiza umuhimu wa kutii hatua zilizopendekezwa za kuzuia msambao wa ugonjwa huo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *