Tume ya Kimataifa ya Majaji tawi la Kenya, ICJ Kenya imetoa wito kwa pande husika katika mgomo unaoendelea wa madaktari nchini kushikiri mazungumzo yatakayosababisha kusitishwa kwa mgomo huo.
ICJ Kenya imelalamikia kuhangaika kwa wagonjwa tangu kuanza kwa mgomo huo ulioitishwa na chama cha madaktari nchini KMPDU Machi 14, 2024.
“Tunatoa wito kwa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), serikali kuu na za kaunti, na KMPDU kukumbatia majadiliano na kusuluhisha masuala yanayoathiri wahudumu wa afya, ambao ni nguzo muhimu katika kufikia haki ya afya kwa Wakenya wote. Pande husika zinapaswa kushiriki meza ya mazungumzo bila masharti na nia nzuri kwa manufaa ya Wakenya wote na maslahi ya wahudumu wa afya,” alisema mwenyekiti wa ICJ Kenya Protas Saende katika taarifa.
“Tunatoa wito kwa SRC, serikali kuu na serikali za kaunti kukiri na kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya, wakiwemo madaktari wanagenzi wanapata malipo bora yanayofungamana na mafunzo yao, utaalam na hali ya kazi yao.”
Kulingana na ICJ Kenya, utoaji wa malipo bora kwa wahudumu wa afya pia utadhibiti hali ya wahudumu hao kutafuta ajira nje ya nchi kama inavyoshuhudiwa kwa sasa licha ya uwekezaji mkubwa unaofanywa katika kutoa mafunzo kwa madaktari, wauguzi, maafisa wa utabibu na wahudumu wengine wa afya.
Wakenya wanaotafuta matibabu wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu tangu kuanza kwa mgomo wa madaktari wiki mbili zilizopita.
Juhudi za serikali kutaka kusitisha mgomo huo zimegonga mwamba baada ya mazungumzo kati yake na madaktari kutibuka mara mbili.
Madakatari wameapa kutorejea kazini hadi matakwa yote 19 yaangaziwe na serikali ikiwa ni pamoja na kutumwa kwa madaktari wanagenzi kuhudumu katika hospitali mbalimbali nchini.