Hospitali zapokea vifaa tiba Vihiga

Alphas Arap Lagat
1 Min Read

Serikali ya kaunti ya Vihiga imesambaza dawa na vifaa vingine vya matibabu vya gharama ya shilingi milioni 38 kwa hospitali zote za umma za kaunti hiyo.

Akizungumza baada ya kuzindua usambazaji huo, Gavana Dkt. Wilber Ottichilo alisema kuwa vifaa hivyo vitasaidia wahudumu wa afya kushughulikia wagonjwa bila ugumu wowote.

Alisema serikali yake imeipa kipaumbele huduma ya afya kwa wote na ataendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa faida ya wakazi.

Dkt. Ottichilo aliipongeza mamlaka ya usambazaji dawa nchini (KEMSA) kwa kufungua kituo kipya jijini Kisumu ambacho kitahudumia eneo la Nyanza na kaunti za magharbi mwa nchi.

“Kufunguliwa kwa kituo cha KEMSA jijini Kisumu kutaongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa vifaa muhimu kwa vitengo vilivyogatuliwa ndani ya eneo linalolengwa,” alisema.

Aliwaonya maafisa wa afya dhidi ya wizi na uuzaji wa dawa akisema watakaopatikana watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Alphas Arap Lagat
+ posts
Share This Article