Hoja ya kumbandua Gachagua: Wakenya watoa maoni

Martin Mwanje
2 Min Read

Cheche kali za kisiasa na wakati mwingine vurugu zilishuhudiwa huku Wakenya katika kaunti zote 47 wakitoa maoni kuhusiana na hoja maalum inayolenga kumfurusha Naibu Rais Rigathi Gachagua madarakani. 

Katika ukumbi wa Bomas, kaunti ya Nairobi, kikao cha utoaji maoni kilisitishwa baada ya vurugu kuzuka ukumbini.

Hii ni hasa baada ya mwanaharakati Morara Kebaso kubebwa hobelahobela na kufurushwa eneo hilo punde alipowasili kutoa maoni yake.

Baadhi ya raia walilalamika vikali wakisema waandaji wa kikao hicho waliwazuia watu waliopinga kutimuliwa kwa Gachagua kutoa maoni.

Katika kaunti ya Nakuru, kikao cha utoaji maoni pia kilitibuka baada ya kuzuka kwa madai kuwa hojaji walizopewa zilikuwa nakala wala si halisi.

Wafuasi wa Gachagua pia walidaiwa kuzuiwa kuingia ukumbini au kutoa maoni, hali iliyosababisha raia kuingia mitaani kulalamikia hali hiyo.

Hoja maalum ya kutaka Gachagua afurushwe kwenye wadhifa huo iliwasilishwa bungeni na mbunge wa Kibwezi Magharibi Eckomas Mwengi Mutuse.

Iliorodhesha mashtaka 11 ikiwa ni pamoja na ukabila na ubadhirifu wa mali ya umma kujitayarisha kama sababu za kutaka Naibu Rais atimuliwe.

Wakenya wameruhusiwa kutoa maoni juu ya hoja hiyo kwa mujibu wa kifungu 118 cha katiba ya nchi.

Jaribio la Naibu Rais jana Alhamisi kutaka mahakama kuzuia zoezi hilo la ukusanyaji maoni ya Wakenya lilishindikana baada ya mahakama kuagiza kuwa kesi hiyo itajwe Oktoba 9 mwaka huu.

Kufikia wakati huo, kesi hiyo huenda ikawa imepitwa na wakati kwani wabunge Oktoba 8 watakuwa wamesikiliza misingi ya mbunge Mutuse kuiwasilisha hoja hiyo na hata kuipigia kura ama kumtimua au kumdumisha Naibu Rais madarakani.

Ikiwa utapitishwa katika Bunge la Taifa, mswada huo pia utapelekwa katika Bunge la Seneti ili kutafuta idhini ya bunge hilo.

Ikiwa pia utapitishwa katika bunge hilo, basi itakuwa rasmi kwamba Naibu Rais ametimuliwa madarakani.

Katika Bunge la Taifa, wabunge 291 walitia saini hoja ya kutaka Gachagua atimuliwe mahakamani.

Ili hoja hiyo ipite katika bunge hilo, wabunge 233 wanahitajika kuiunga mkono hoja hiyo.

Share This Article