Chama cha ODM kimekanusha madai kuwa kinafanya mazungumzo na utawala wa Kenya Kwanza kwa nia ya kuunda serikali ya muungano.
Chama hicho badala yake kinasema mwanachama yeyote atakayeridhia kuteuliwa kama waziri au kwenye wadhifa wowote serikalini atafanya hivyo kwa hiari yake.
“Kama chama, tungependa kuelezea wazi kwamba hatufanyi mazungumzo na utawala wa Ruto wa kujiingiza katika mpangilio wowote wa muungano au wa kisiasa,” amesema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna katika taarifa leo Jumanne.
“Mwanachama yeyote wa ODM atakayeridhia kujiunga na Baraza la Mawaziri la Kenya Kwanza au wadhifa mwingine wowote atafanya hivyo bila kibali au kuungwa mkono na chama.”
Huku kikielezea kuunga mkono maandamano ya vijana wa Gen Z yanayolenga kushinikiza kutekelezwa kwa mabadiliko nchini, chama hicho kimesisitiza haja ya kufanya mazungumzo jumuishi na ya kweli ya kitaifa yenye lengo la kusulushisha changamoto si haba inazokumbana nazo nchi hii.
Hata hivyo, kulingana na ODM, mazungumzo hayo yanapaswa kutanguliwa na kutimizwa kwa masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzilipa fidia familia za waliouawa wakati wa maandamano, kuachiliwa kwa watu wote waliokamatwa na kutupiliwa mbali kwa kesi dhidi yao, kushtakiwa kwa polisi wanaotuhumiwa kwa kuua waandamanaji na kufutwa kazi kwa Kamanda wa Polisi wa Nairobi Adamson Bungei.
Matamshi ya ODM hasa kuhusu serikali ya muungano yanakuja wakati ambapo uvumi umetokota kwamba kiongozi wa chama hicho Raila Odinga amefikia makubaliano na Rais Ruto ya kuunda serikali ya muungano.
Rais Ruto ametangaza orodha ya kwanza ya Baraza Jipya la Mawaziri na orodha nyingine inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Kumekuwa na makisio kwamba orodha hiyo huenda ikawajumuisha wanachama wa ODM.