Mwanamuziki wa Tanzania Rajab Abdul Kahali, maarufu kama Harmonize ametangaza kwamba atazindua albamu yake ya tano mwezi huu.
Albamu hiyo iliyopatiwa jina “Muziki wa Samia” itazinduliwa rasmi Mei 25, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.
Harmonize alisema kwamba lengo kuu la kazi hiyo ya sanaa ni kutambua kazi nzuri anayoendelea kufanya Rais Samia Suluhu Hassan katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Mwanamuziki huyo alisema pia kwamba albumu hiyo ndiyo yake ya mwisho huku akisisitiza kwamba ameimba sana kuliko kawaida. Alifichua pia kwamba ina nyimbo 10 ambazo zote zinamhusu Rais Samia.
Baada ya albamu hiyo anasema atachukua mapumziko na kisha kuanza kutoa nyimbo moja moja na wala sio mkusanyiko katika albamu.
Watakaohudhuria hafla hiyo ni wale ambao watakuwa wamealikwa pekee na kwamba hakutakuwa na ada ya kuingia.
aliahidi onyesho la kipekee siku hiyo kwani amekusanya mazuri yote ambayo yanafanywa na Rais Samia na Serikali na kuyaweka kwenye kitabu kimoja cha kumbukumbu ambacho kitaishi milele kiitwacho “Muziki wa Samia”.