Harambee Stars yaporomoka nafasi nne katika uorodheshaji wa FIFA

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu ya taifa ya Harambee Stars imeshuka kwa nafasi nne kutoka nambari 105 hadi 109 katika uorodheshaji wa dunia wa FIFA wa mwezi Septemba uliotangazwa Alhamisi.

Kenya iliishinda Qatar mabao 2-1  na kupigwa na Sudan Kusini goli moja kwa nunge kwenye michuano miwili ya kirafiki iliyocheza mwezi Septemba.

Barani Afrika, Harambee Stars inakalia nafasi ya 25.

Atlas Lions ya Morocco imechupa kileleni Barani Afrika ikishikilia nafasi ya 13 ulimwenguni, ikifuatwa na mabingwa wa Afrika Simba wa Teranga kutoka Senegal walioshuka hadi nafasi ya 20, wakifuatwa na Tunisia katika nambari ya 29 wakati Algeria na Misri zikifuatana katika nafasi za 34 na 35 ulimwenguni.

Nigeria ni ya 40 na ya 6 Afrika, Cameroon ya 41, Mali ya 49 wakati Ivory Coast na Burkina Faso zikihitimisha nafasi za 9 na 10 mtawalia.

Nafasi saba bora ulimwenguni hazina mabadiliko yoyote, mabingwa wa dunia Argentina wakiongoza wakifuatwa na Ufaransa, Brazil ni ya tatu, Uingereza ya nne nayo Ubelgiji ni ya tano.

Croatia inashikilia nafasi ya 6 ikifuatwa na Uholanzi iliyo ya saba wakati Ureno ikikwea hadi nambari nane nayo Italia ikashuka hadi nafasi ya 9 kisha Uhispania imedata katika nafasi ya kumi duniani.

Share This Article