Timu ya taifa ya soka ya Kenya kwa wanawake – Harambee Starlets, ilisajili ushindi mkubwa wa kihistoria baada ya kuidhalilisha Ushelisheli magoli 11-0 katika mkondo wa kwanza raundi ya kwanza kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki mwaka 2028.
Mchuano huo ulipigwa Alhamisi alasiri katika uchanjaa wa Ulinzi. Starlets walikuwa kifua mbele kwa magoli 3-0 kufikia muda wa mapumziko kupitia kwa mabao ya Valary Nekesa aliyepachika mawili na Elizabeth Muteshi.
Hali ilikuwa tete kipindi cha pili kwa wageni huku Muteshi akiongeza bao dakika ya 54, kabla ya Alrin Madalina kutikisa nyavu mara mbili kufanya mambo kuwa 6-0 dakika ya 82.
Dakika moja baadaye, Martha Amunyolete alitanua uongozi kwa bao la saba nao Mercy Airo na Elizabeth Mideva wakaongeza mawili kila mmoja.
Pambano la marudio litaandaliwa katika uwanja wa Ulinzi Oktoba 12 huku mshindi akikutana na aidha Malawi au Zimbabwe kwenye raundi ya pili.