Rais William Ruto, ameelezea kujitolea kwa serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, licha ya changamoto zilizoghubika utekelezwaji wa hazina ya bima ya afya ya jamii SHIF.
Akizungumza alipohutubia kikao cha pamoja cha bunge la taifa na lile la Senate leo Alhamisi, kiongozi huyo wa taifa alisema serikali imechukua hatua muhimu za kuimarisha mfumo wa huduma za afya hapa nchini.
Alidokeza kuwa katika muda wa mwezi mmoja uliopita, shilingi bilioni tano zimetolewa kulipa madeni katika ituo vya afya vya umma, vile vya kibinafsi na vinavyomilikiwa na taasisi za kidini, huku shilingi zingine biliono 3.7 zikiratibiwa kutolewa siku za Ijumaa.
“Sawia na aina nyingine za mpito, kuna changamoto, lakini tumejitolea kuhakikisha mfumo huu unafanya kazi,” alisema Rais Ruto.
Hadi kufikia sasa, Rais Ruto alisema zaidi ya wakenya milioni 15 wamejisajili kwa hazina ya bima ya afya SHIF, ambao sasa unajulikana kama Taifa Care.
“Mara tu mpito kutoka iliyokuwa hazina ya taifa ya bima ya afya NHIF hadi ile ya SHIF utakapokamilika, Kenya itakuwa na mfumo wa afya ambao unahakikisha maadili na usawa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kila mmoja kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 60 tangu taifa hili lipate uhuru,” aliongeza Rais Ruto.
Alisema mpango huo mpya wa afya utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya, huku serikali ikihudumia wananchi walio katika mazingira magumu na umaskini.