Hakuna kisa kingine cha Mpox kimeripotiwa nchini, asema Waziri Barasa

Martin Mwanje
1 Min Read

Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa amewahakikishia Wakenya kuwa hakuna kisa kingine cha ugonjwa wa Mpox ambacho kimeripotiwa nchini. 

Hii ni tangu kupona kwa mgonjwa wa kwanza ambaye aliripotiwa kuambukizwa ugonjwa huo Julai 29 mwaka huu.

Mgonjwa huyo alikuwa amesafiri kutoka mjini Kampala nchini Uganda hadi mjini Mombasa na kisha nchini Tanzania kupitia Taita Taveta akielekea nchini Rwanda.

“Tumewapima watu 12 waliotangamana na mgonjwa huyo na watu wengine sita walioshukiwa kuambukizwa ugonjwa huo na wote wamebainika kutoambukizwa,” amesema Waziri Barasa katika taarifa.

“Hakuna kisa kingine kipya cha ugonjwa wa Mpox kimeripotiwa kutokea nchini tangu kuthibitishwa kwa kile cha kwanza.”

Barasa amesema wizara yake imeweka hatua za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuongeza uangalizi, kutoa ushauri kwa wahudumu wa afya kwa lengo la kuwahamasisha juu ya ugonjwa wa Mpox, kuuelimisha umma na kutoa tahadhari kuhusiana na ugonjwa huo miongoni mwa hatua zingine.

Shirika la Afya Duniani, WHO limeutangaza ugonjwa wa Mpox kuwa dharura ya afya ya umma ambayo inaibua mashaka duniani.

Share This Article