Hafla ya kumuenzi Gatwiri kuandaliwa leo

Marion Bosire
2 Min Read

Kamati andalizi ya mazishi ya muunda maudhui mitandaoni Tabitha Gatwiri pamoja na falimia yake wametangaza kwamba hafla ya kumuenzi itaandaliwa jioni ya leo.

Hafla hiyo iliratibiwa kuanza saa tisa jioni leo hadi baadaye katika hoteli ya Blue Springs ambayo iko kwenye barabara kuu ya Thika.

Familia ya mwendazake pia inaomba usaidizi wa kifedha ili kumpa mazishi faafu ambapo michango inatumwa kupitia jukwaa la M-Changa.

Kakake Gatwiri aitwaye Brian Kirimi naye ametoa nambari ya simu ambayo ni 0112843595 kwa mawasiliano kuhusu mipango ya kumpumzisha dadake.

Mwili wa mwendazake utazikwa nyumbani kwa babake huko Meru, Ijumaa Novemba 15, 2024.

Hafla ya mazishi kulingana na tangazo la awali itakuwa katika kituo cha utamaduni cha Thiiri kwenye barabara kuu ya kutoka Meru kuelekea Ruiri kuelekea Isiolo, karibu na soko la Mugene.

Baada ya mkutano na ibada ya mazishi, mwili wa Gatwiri utazikwa nyumbani kwa babake, umbali wa kilomita kama moja hivi kutoka eneo la mkutano.

Mwili wa Gatwiri uligunduliwa kwenye nyumba yake ya kupangisha yapata wiki moja iliyopita na kakake ambaye aliamua kumzuru baada yake kukosa kujibu jumbe zake na hata kukosa kuchukua simu.

Uchunguzi wa maiti yake uliofanyika katika makafani ya hospitali ya chuo kikuu cha Kenyatta ulibaini kwamba aliaga dunia kwa kushindwa kupumua ipasavyo kutokana na namna alikuwa amelala.

Share This Article