Gitaa iliyopasuliwa na kuundwa tena kuuzwa mnadani

Gitaa hiyo ya mwanamuziki Kurt Cobain wa bendi ya Nirvana iliundwa tena baada yake kuipasua na hivyo inaweza kutumika tena.

Marion Bosire
2 Min Read

Gitaa ya mwanamuziki Kurt Cobain ambayo alipasua wakati wa ziara ya kikazi ya bendi ya Nirvana ya Uingereza mwaka 1992 itauzwa kwenye mnada.

Mnada wa ala hiyo ya muziki aina ya Fender Stratocaster unatarajiwa kufunguliwa rasmi Jumatano, Aprili 9, 2025 na bei ya kuanzia ni dola elfu 30.

Hatua hii huenda ikawafurahisha mashabiki wa bendi ya Nirvana, ambao wamealikwa kushiriki mnada huo ili kujipatia ala ya mwanamuziki waliyempenda sana.

Ala hiyo hata hivyo ilifanyiwa marekebisho makubwa na ukarabati ili kuirejesha katika hali ya kuweza kutumika tena.

Jamaa mmoja ambaye alifanya kazi kama msaidizi wa bendi ya Nirvana kati ya mwaka 1991 na 1993 ndiye alinunua ala hiyo ambayo Kurt alimiliki binafsi ambayo huchezwa kwa mkono wa kushoto.

Baada ya kuiunda na kuikarabati, aliipeleka kwa John Duncan mtaaamu wa ala za gitaa wa muda mrefu wa bendi ya Nirvana kwa ajili ya ukaguzi, kama njia ya kuhakikishia umma uhalisia wake.

Gitaa nyingine ya Kurt aina ya Fender Stratocaster aliyopasua pia iliuzwa kwa zaidi ya dola nusu milioni mwaka 2023, huku nyingine iliyoundwa mwaka 1969 ya rangi ya samawati ikuzwa kwa dola milioni 4.5.

Mnada huo wa gitaa utaendeshwa mitandaoni na unajiri siku chache tu baada ya maadhimisho ya miaka 31 tangu alipofariki Kurt.

Kurt alikata roho baada ya kupigwa risasi Aprili 5, 1994 akiwa na umri wa miaka 27.

Mazingira ya kifo chake hata hivyo yameghubikwa na utata huku wengi wakikisia kwamba aliuawa lakini ripoti ya uchunguzi wa maiti yake, iliyovujishwa iliashiria kwamba alijitoa uhai.

Ripoti hiyo ya mtaalamu wa uchunguzi Tom Grant iliyosambaa mwaka jana ilidai kwamba Kurt alikuwa ameacha ujumbe kwenye makazi yake kabla ya kujiua huku akipatikana na bastola kwenye mkono wake wa kushoto.

Kurt Cobain, mwimbaji mkuu wa bendi ya Nirvana alikuwa na desturi ya kupasua ala za muziki wakati wa matamasha.

Website |  + posts
Share This Article