Ghasia zinasemekana kuendelea kuongezeka nchini Ufaransa pale ambapo waandamanaji ambao wengi ni wa umri mdogo walikimbizana na maafisa wa polisi usiku wa Jumamosi Juni, 1. Maafisa hao wanaripotiwa kutia mbaroni waandamanaji wapatao 700 katika miji mbali mbali nchini Ufaransa usiku.
Chachari hizo zinatokana na kisa cha mvulana mmoja wa asili ya kaskazini ya Afrika kuuawa na maafisa wa polisi na zilianza punde baada ya mazishi yake.
Nahel M wa umri wa miaka 17 ambaye wazazi wake ni wa asili ya Algeria na Morocco alipigwa risasi na afisa wa polisi katika eneo la Nanterre Jumanne. Kisa hicho ambacho kilinakiliwa kwenye video kimesababisha kuhuishwa kwa lalama za jamii zisizo asilia nchini Ufaransa kuhusu ubaguzi wa maafisa wa polisi.
Mwendesha mashtaka mmoja wa Nanterre alisema mahakamani Alhamisi kwamba Nahel alikuwa na tabia ya kukosa kutii maagizo ya maafisa wa trafiki barabarani ya kusimamisha gari na alikuwa akiendesha gari la kukodisha kinyume cha sheria.
Waandamanaji wa Jumamosi usiku walilenga makazi ya Meya wa jiji la Paris ambapo waligongesha gari kwenye lango la kuingia na kuwasha moto. Meya huyo kwa jina Vincent Jeanbrun alielezea kupitia Twitter kwamba mke wake na mwanawe mmoja waliumia kwenye purukushani hiyo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa amepangiwa kuanza ziara ya kikazi nchini Ujerumani leo Jumapili lakini ameahirisha ili kushughulikia tatizo hilo la ulinzi. Huu ndio mgogoro mbaya zaidi ambao umetokea wakati wa uongozi wa Macron tangu maandamano ya “Yellow Vest” ya mwaka 2018 ambayo yalilemaza ulinzi na utulivu kote nchini humo.