Gavana wa zamani wa kaunti ya Nyandarua Daniel Waithaka Mwangi na Waziri wa Maji wa zamani wa kaunti hiyo Grace Wanjiru Gitonga wamehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kila mmoja au walipe faini ya shilingi milioni moja.
Hii ni kutokana na kuhusuika kwao katika sakata ya utoaji zabuni ya shilingi milioni 50.
Wawili hao walipatikana na hatia Machi 13, 2025 kuhusiana na mashtaka mbalimbali yanayohusiana na ufisadi.
Waithaka alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Evans Keago mjini Nyahururu akikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kutii sheria za kufanya manunuzi.
Leo Alhamisi, Machi 20, 2025, Gavana huyo wa zamani alihukumiwa miaka miwili jela kwa kila shtaka au alipe faini ya shilingi milioni moja.
Wakati huohuo, Gitonga pia alihukumiwa kwa mashtaka mawili ya kushindwa kuzingatia sheria za manunuzi na kuanzisha mradi bila mpangilio wa awali. Naye pia amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kila shtaka au alipe faini ya shilingi milioni moja.
Mahakama itaandaa kikao Machi 24, 2025 ili kubaini ikiwa faini hizo zimelipwa au washtakiwa wataanza kutumikia vifungo vyao.