Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti atuzwa na Benki ya Dunia

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti atuzwa.

Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti ametuzwa kwa utekelezaji bora wa mradi wa kilimo wa mabadiliko ya tabia nchi KCSAP, unaofadhiliwa na benki ya dunia.

Benki ya dunia iliorodhesha kaunti ya Machakos ya tatu hapa nchini, kati ya kaunti 24 ambazo zinatekeleza mradi huo wa KCSAP, kwa lengo la kuboresha maisha ya wakazi kupitia mbinu bora za kilimo.

Akizungumza afisini mwake alipopokea tuzo hiyo, Wavinya alisema serikali yake imejitolea kuimarisha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo, na tuzo hiyo ni ishara tosha kwamba anaunga mkono jamii zinazoishi katika kaunti hiyo.

Kupitia ushirikiano na mpango huo wa KCSAP, serikali ya kaunti ya Machakos imekarabati mabwawa matano, ambayo ni pamoja na  Ukanga Utune (Kangundo),  Kilaata (Ikombe)  Kithaayoni (Kalama), Limba (Wamunyu) na Kitambaasye (Matungulu) kwa kitita cha shilingi Milioni 83.

“Athari za miradi iliyotekelezwa kupitia mpango wa  KCSAP, itashuhudiwa na vizazi vijavyo, na serikali yangu imejitolea kutatua  na changamoto zinazowakabili wakazi wa kaunti hii,” alisema Wavinya.

Kulingana na Gavana huyo, jumla ya vikundi 382 vimenufaika pakubwa na ufadhili mbali mbali katika kuanzisha miradi mbali mbali ikiwemo uzalishaji mbegu, chakula cha kuku, kilimo miongoni mwa mingine.

“Lengo letu kuu ni kuhakikisha kuna chakula cha kutosha katika kaunti ya Machakos na kuboresha maisha ya wakazi wetu,” aliongeza Wavinya.

Tuzo hiyo iliwasilishwa kwake na mshirikishi wa kitaifa wa mradi huo wa KCSAP Priscah Muiruri kutoka kwa wizara ya kilimo, huku akimpongeza Gavana Wavinya kwa kuwa na uwazi wakati wa kutekeleza miradi ya  KSCAP.

Share This Article