Gavana Sakaja ashikilia kuwa wafanyabiashara wa Marikiti watahamishwa

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Saa chache baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kukutana na wafanyabiashara katika masoko ya Nairobi, na kumtaka Gavana Sakaja kushiriki meza ya mazungumzo kabla ya kuwahamisha, Gavana huyo ameshikilia kuwa lazima wafanyabiashara hao wahamishwe.

Huku akimjibu Naibu huyo wa Rais, Gavana Sakaja alisema baadhi ya wafanyabiashara hao wanahatarisha maisha yao kwa kufanya biashara kando kando ya barabara, swala ambalo serikali yake haitavumilia.

“Serikali yangu haina mipango ya kuhamisha soko la Marikiti. Baadhi ya bidhaa zitasambazwa kwa jumla katika masoko mengine yaliyojengwa na fedha kutoka kwa ushuru. Kile ambacho hatutakubali ni wafanyabiashara kuhatarisha maisha yao kwa kuuza bidhaa kando kando ya barabara. Watahamishwa hadi soko lililoko katika barabara ya Kangundo,” alisema Sakaja.

Gavana alitoa mfano wa ajali iliyotokea Londiani na kusababisha vifo vya wafanyabiashara 52 na wengine wengi kupata majeraha mabaya, akisema kuwa anajukumu la kutekeleza la kulinda maisha.

Kuhusu wito wa Gachagua kwa Sakaja, kwamba ashauriane na wafanyabiashara hao kabla ya kuchukua hatua yoyote, Gavana huyo alifafanua kuwa amekuwa akishirikiana na na viongozi na wafanyabiashara wa masoko ya Marikiti na wakulima na wanakubaliana na hatua hiyo.

“Umesema nishauriane na wafanyabiashara walioathiriwa. serikali yangu imeshaurian na viongozi wa soko la Wakulima/Marikiti wiki iliyopita. Tulikubaliana kuhusu hatua hii na maswala mengine kuboresha usalama na maslahi ya wanaviashara hao. hatutakubali uturudishe nyuma,” alidokeza Sakaja.

Awali wafanyabiashara wa soko la Marikiti/Wakulima waliandamana kupinga kuhamishwa kwao hadi kwa soko lililoko katika barabara ya Kangundo.

Website |  + posts
Share This Article