Kaunti ya Makueni imezindua mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa afya wa hali ya juu unaoitwa “Afya Makueni” unaolenga kuboresha huduma za afya kwa wakazi.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu na kuongozwa na Gavana Mutula Kilonzo Jr katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Makueni, MCRH.
Kilonzo ameitaja hatua hiyo kuwa muhimu katika sekta ya afya ya kaunti hiyo.
Mfumo huo mpya unachukua nafasi ya taratibu za zamani za kutumia karatasi ambazo hazikuwa na ufanisi na ziliendeshwa kwa mifumo iliyojitegemea na isiyo wazi.
Mpango huo unalingana na ajenda ya utawala wa Gavana Kilonzo ya uwekaji wa mifumo inayojiendesha na ya kidijitali kama ilivyobainishwa katika mipango ya maendeleo ya kaunti, CIDP ya 2023-27.
Alielezea “Afya Makueni” kama juhudi za msingi zilizoanzishwa ili kuleta mapinduzi katika usimamizi na utoaji wa huduma za afya katika kaunti.
Mfumo huo unatarajiwa kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya huduma za dawa na zisizo za dawa zinazotolewa na vituo vya kaunti.
Dkt. Paul Musila, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Afya ya Kaunti, alieleza kuwa mfumo huo mpya utaunganisha vituo vyote vya afya, kuhakikisha mtiririko mzuri wa habari ili kuboresha huduma kwa wagonjwa, kurahisisha shughuli na kuongeza ufanisi kwa ujumla.
Alisisitiza kwamba hatua ya kuelekea mazingira yasiyotumia karatasi itasababisha taratibu za kiutawala kuwa bora zaidi na kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa.
Baada ya kutekelezwa kikamilifu, mfumo wa kati utaondoa hitaji la wagonjwa kujiandikisha mara kadhaa katika vituo tofauti. Kwa mfano, mgonjwa aliyesajiliwa Mtito Andei hatahitaji kujiandikisha tena katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Makueni (MCRH) au kituo kingine chochote.
Aidha, mfumo huo utatoa mtazamo wa kina wa historia ya wagonjwa, ikiwa ni pamoja na matibabu ya awali, dawa na mizio ili kusaidia katika utambuzi bora na mipango ya matibabu.
Zaidi ya hayo, mfumo huo utawezesha vituo vya afya kubadilishana bidhaa za afya, hivyo kuboresha matumizi ya rasilimali na utoaji wa huduma katika kaunti nzima.
Mradi huo ni unatekelezwa kwa pamoja na idara za ICT na afya, ukionyesha juhudi za ushirikiano kwa lengo la kuboresha huduma za afya katika kaunti ya Makueni.