Gavana Kihika aitwa kuhudhuria kikao katika seneti

Marion Bosire
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Nakuru Susan Kihika ameitwa kuhudhuria kikao cha kamati ya bunge la seneti kuhusu Afya, kutokana na mzozo unaoendelea wa hospitali ya War Memorial.

Ikiwa miezi miwili imepita sasa huduma zikiwa zimelemazwa katika taasisi hiyo ya afya, kamati ya Afya imeamua kuita wahusika wote ili waonyeshe stakabadhi za umiliki wake.

Haya yanafuatia mvutano kati ya serikali ya kaunti ya Nakuru na usimamizi wa hospitali hiyo ambapo kaunti inalaumiwa kwa kupuuza maagizo sita kutoka kwa mahakama.

Jaji mkuu Martha Koome wiki jana alikashifu serikali ya kaunti ya Nakuru kwa kuendelea kupuuuza maagizo ya mahakama ilipobainika kwamba majaji wanaohusika na kesi hiyo wametishiwa.

Seneta wa kaunti ya Nakuru Tabitha Karanja Keroche, anasema nia ya kamati hiyo ya Afya katika bunge la Seneti ni kupata habari kutoka kwa pande zote.

Karanja alikuwa amewasilisha ombi kwa bunge la Seneti kuingilia kati suala hilo baada ya serikali ya kaunti kutwaa hospitali hiyo ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa wa figo.

Website |  + posts
Share This Article