Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ameondolewa mamlakani baada ya bunge la Seneti kudumisha kung’atuliwa kwake na bunge la kaunti ya Meru.
Bunge la Seneti jana Jumanne usiku lilimpata Gavana huyo na hatia dhidi ya mashtaka matatu aliyokabiliwa nayo.
Mashtaka dhidi ya Mwangaza yalikuwa ni pamoja na ukiukaji wa katiba, utumizi mbaya wa mamlaka na utovu wa maadili.
Katika shtaka la kwanza la ukiukaji katiba, Maseneta 26 walipiga kura kuwa Mwangaza ana hatia huku wanne wakisema hana hatia. Maseneta 14 hawakupiga kura.
Katika shtaka la pili la utovu wa maadili, Maseneta 26 walisema ana hatia na wanne kusema hana hatia.
Na katika kosa la tatu la utumizi mbaya wa mamlaka, Maseneta 27 walipiga kura kusema ana hatia na Seneta mmoja kupiga kura kupinga kosa hilo.
“Kuambatana na sura ya 181 ya katiba, sehemu ya 33 ya serikali za kaunti na kanuni za bunge nambari 86 ya bunge la Seneti, bunge la Seneti limeazimia kumuondoa mamlakani Gavana wa Meru Kawira Mwangaza,” alitangaza spika wa bunge hilo Amason Kingi.
Mwangaza ambaye alihudhuria vikao vya bunge hilo vya kusikiliza mashtaka dhidi yake, alikuwa amekanusha mashtaka hayo yaliyowasilishwa na bunge la kaunti ya Meru.
Awali, Gavana huyo alinusurika majaribio mawili ya kumuondoa mamlakani, jaribio la kwanza likiwa mwezi Disemba mwaka 2022 na la pili likiwa mwezi Novemba mwaka 2023.