Gavana Guyo mashakani, Seneti yaamrisha polisi kumkamata

Tom Mathinji
1 Min Read
Amason Kingi - Spika wa Bunge la Seneti

Gavana wa kaunti ya Isiolo Abdi Ibrahim Hassan amejipata mashakani, baada ya spika wa bunge la Senate Amason Kingi, kutoa agizo kwa Inspekta Jenarali wa polisi Douglas Kanja, kumkamata Gavana huyo na kumwalisha katika bunge la Senate.

Akitoa agizo hilo wakati wa vikao vya bunge leo Jumanne, Kingi alisema Gavana huyo amekiuka maagizo kadhaa ya kufika mbele ya bunge hilo, kujibu maswala yaliyoibuliwa na kamati kadhaa za Senate.

“Gavana Abdi Ibrahim Hassan, amefeli mara kadhaa kufika mbele ya kamati kadhaa za bunge la Senate, baada ya kualikwa au kuagizwa kufanya hivyo,” alisema Spika Kingi.

Kingi alitoa mfano ambapo Gavana huyo alikosa kutii magizo kadhaa ya kufika mbele ya wa kamati ya uhasibu wa fedha za umma, PAC.

Vile vile spika huyo alisema Gavana huyo alikosa kufika mbele ya kamati ya fedha na bajeti na pia alikosa kufika mbele ya kamati ya bunge hilo kuhusu Afya.

Aidha Gavana huyo anadaiwa kutumia matamshi yasiyofaa kwa wanachama wa kamati ya uwekezaji wa umma na fedha maalum.

Arifa ya hoja tayari imewasilishwa katika bunge la seneti kujadilia mienendo ya Gavana huyo, huku likitishia kusimamisha ugavi wa pesa kwa serikali ya kaunti hiyo hadi pale Gavana huyo atakapowajibika.

Share This Article