Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani amewahimiza wanafunzi waliokamilisha masomo ya darasa la nane na kufeli mtihani wa KCPE kujiunga na vyuo vya kiufundi katika kaunti hiyo ili kujipatia ujuzi utakaowasaidia maishani.
Kufikia sasa, kaunti ya Kwale imejenga jumla ya vyuo vya kiufundi 43 katika kaunti hiyo vinavyotoa mafunzo ya kiufundi mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ujenzi, useremala, utengezaji magari, mafunzo ya urembo pamoja na mafunzo ya uchumi baharini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa chuo cha kiufundi cha Kingwende, Achani amesema kuwa serikali imetoa ruzuku ya shilingi milioni 10 kufadhili masomo ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya kiufundi ambapo kila mwanafunzi atalipiwa shilingi elfu 12 pindi atakapojiunga na vyuo hivyo.
Alielezea kutamaushwa kwake na idadi ndogo ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya kiufundi katika kaunti ya Kwale, idadi hiyo ikifikia wanafunzi elfu 4 pekee na kuwataka wazazi kujukumika.
Kauli iliyoungwa mkono na Mwakilishi Wadi wa Ramisi Hanifa Mwajirani na Naibu Kamishna wa Kwale eneo la Msambweni Denis Juma waliowataka wazazi kutilia maanani masomo ya watoto wao.