Gavana wa Kaunti ya Kwale Fatuma Achani siku ya Jumamosi ametoa hundi za msaada wa masomo za jumla ya shilingi milioni 400 kupitia mpango wa ‘Elimu ni Sasa’ katika uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Ukunda eneo la Msambweni.
Mpango huo unalenga kufadhili masomo ya wanafunzi 17,790 wa shule za upili na vyuo vikuu, wengi wakiwa wale wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo, kutoka wadi zote 20 za kaunti ya Kwale.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Gavana Achani amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa watoto wale hawakosi masomo kutokana na ukosefu wa karo.
Achani amedokeza kuwa, tangu kubuniwa kwa mpango huo wa Elimu ni sasa, mwaka 2013, wanafunzi 16,000 wa shule za upili na 6,000 wa vyuo vikuu wamenufaika.