Gachagua: Vita dhidi ya Pombe haramu na mihadarati vimefaulu

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, amesema mikakati iliyowekwa kukabiliana na pombe haramu na mihadarati imezaa matunda, huku maelfu ya vijana wakiokolewa.

Akizungumza Ijumaa afisini mwake mtaani Karen alipoandaa mkutano wa kuangazia hatua zilizopigwa dhidi ya pombe haramu na mihadarati, naibu huyo wa Rais alisema serikali iliunga mkono kikamilifu utekelezwaji wa hatua hizo.

“Tumefanya vyema zaidi. Nawapongeza nyote kwa hatua  mlizochukua kupiga jeki juhudi za serikali. Kumekuwa na ushirikiano bora kati ya asasi mbali mbali,” alisema Gachagua.

Gachagua alisema ripoti kutoka pembe zote za nchi, zinaashiria kuwa uuzaji wa pombe haramu umepungua, huku akiahidi kuendeleza hatua za kutokomeza matumizi hayo kabisa.

“Mambo sasa ni mazuri. Tutaendelea kushirikiana ili kuchunguza hatua zilizopigwa katika vita hivi,” aliongeza naibu huyo wa Rais.

Mkutano huo ulihudhuriwa na waziri wa biashara Rebecca Miano, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, mwakilishi wa idara ya Mahakama  Ase Opondo na katibu katika wizara ya afya Mary Muthoni miongoni mwa viongozi wengine.

Website |  + posts
Share This Article