Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema serikali ya kitaifa inaratibu mipango ya kustawisha kaunti ya Nairobi, kwa lengo la kudumisha hadhi ya jiji kuu hili la Kenya.
Akizungumza leo Jumamosi katika hafla ya kuchangisha fedha kwa mpango wa kuwawezesha Wanawake katika eneo bunge la Langata katika uwanja wa michezo wa Nyayo Jijni Nairobi, Gachagua alisema Jiji hili ni muhimu na kamwe halipaswi kutelekezwa.
“Nitachukua hatua kabambe kustawisha kaunti ya Nairobi kwa kuwa ni Jiji kuu la Kenya na kitovu cha serikali. Ni kituo cha kibiashara cha Afrika Mashariki na kati. Mimi pamoja na Rais tutahakikisha kila kitu kiko shwari katika jiji hili,” alidokeza Gachagua.
Gachagua alisema Nairobi ni muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Tunapaswa kurejesha hadhi ya Jiji la Nairobi na kuhakikisha wakazi wanapata huduma wanazohitaji. Sisi sote ni wadau katika Jiji hili,” alisema naibu huyo wa Rais.
Aidha, alisema uongozi wa nchi umeazimia kushirikiana na viongozi wote bila kujali miegemeo yao ya kisiasa ili kuhakikisha jiji la Nairobi linarejesha hadhi yake.
“Tutafanya kazi na viongozi wote bila kujali miegemeo yao ya kisiasa. Huu ni wakati wa kuwahudumia wakenya,” alisema Gachagua.
Gachagua alikuwa ameandamana na wabunge kadhaa katika hafla hiyo.