Naibu Rais Rigathi Gachagua aliyebanduliwa kwenye wadhifa huo na Bunge la Seneti atafahamu hatima yake kesho Alhamisi.
Hii ni pale jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu litakapotoa uamuzi wake juu ya ikiwa lifutilie mbali maagizo yaliyotolewa awali na mahakama ya kuzuia kubanduliwa kwake.
Ikiwa majaji Fred Ogola, Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi wataondoa maagizo hayo, basi hatua hiyo itapisha kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki.
Upande wa washtakiwa, ikiwa ni pamoja na serikali kuu kupitia Mwanasheria Mkuu, Bunge la Taifa na lile la Seneti, unashinikiza maagizo hayo kuondolewa ili kupisha kuapishwa kwa Prof. Kindiki.
Kwa kufanya hivyo, hatua hiyo itaondoa ombwe la kisiasa lililopo nchini kwa sasa.
Kwa upande wake, Gachagua anataka maagizo kudumishwa hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.
Majaji hao wanatarajiwa kutoa uamuzi juu ya maagizo hayo kesho Alhamisi, majira ya saa 8:30 alasiri.