Naibu Rais Rigathi Gachagua ameyahakikishia mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohudumu hapa nchini, kuwa serikali imeimarisha ushirikiano wake katika kuhakikisha utekelezwaji wa malengo ya maendeleo ya mashirika hayo.
Naibu huyo wa Rais alisema utawala wa Rais William Ruto, utaendelea kushirikiana na kufanya kazi na mashirika hayo 24 ya Umoja wa Mataifa katika miradi ya pamoja ya maendeleo.
Akizungumza leo Jumatano wakati wa mkutano wa ushirikiano kati ya Kenya na Umoja wa Mataifa katika makazi ya naibu Rais mtaani Karen, Jijini Nairobi, Gachagua alisema kuna uhusiano katika majukumu ya Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa na mpango wa serikali wa kuimarisha uchumi almaarufu Bottom-Up Economic Transformation Agenda (BETA).
“Niapongeza Umoja wa Mataifa kwa mipango yake ya pamoja inayotekelezwa na wizara za serikali,” alisema Gachagua.
Kwa upande wake, mshirikishi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini Dkt. Stephen Jackson, alisema mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini yamewiainisha miradi ya maendeleo na nguzo za mpango wa kuimarisha uchumi wa Bottom-Up Economic Transformation Agenda (BETA)
Mkutano huo wa Jumatano uliandaliwa kupigia kurunzi ufanisi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini wa mwaka 2023 na mipangilio ya mwaka 2024.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na waziri wa mazingira na misitu Soipan Tuya, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, katibu katika baraza la mawaziri Mercy Wanjau, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Makatibu wa wizara Ann Wang’ombe (Jinsia), Hillary Kimtai (Huduma za matibabu), Teresia Mbaika (Ugatuzi) na James Muhati (Mipango ya Uchumi).