Gachagua awataka wabunge kupitisha mswada wa kahawa haraka

Marion Bosire
1 Min Read

Aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, amewataka wabunge watumie kasi waliyotumia kumbandua madarakani, kupitisha mswada wa Kahawa wa mwaka jana.

Gachagua alikuwa akihutubia umati uliokuwa ukihudhuria mazishi huko Gichugu katika kaunti ya Kirinyaga ambapo alisema wabunge hasa wa eneo la mlima Kenya wanafaa kuhakikisha serikali inalipa madeni inayodaiwa na wakulima.

Rigathi Gachagua vile vile aliapa kumpatia kiongozi wa nchi fursa ya kufanya kazi kwa muda uliosalia muhula huu licha ya kung’atuliwa madarakani hivi maajuzi.

Alisema wakazi wa eneo la Mlima Kenya wako tayari kumpa Rais William Ruto muda wa kutimiza ahadi alizotoa kwao.

Siku moja tu baada ya Profesa Kithure Kindiki kuapishwa kuchukua mahala pake, Gachagua alisema haweki lolote moyoni kutokana na yaliyompata kupitia kubanduliwa afisini na bunge la kitaifa na bunge la seneti.

Hiyo ndiyo mara ya kwanza Gachagua, alizungumza kwa umma tangu kung’atuliwa mamlakani huku akimshauri Rais Ruto amkabidhi mrithi wake baadhi ya majukumu aliyokuwa akitekeleza.

Majukumu hayo ni pamoja na utetezi wa mtoto wa kiume pamoja na vita dhidi ya pombe haramu.

Share This Article