Klabu ya AFC Leopards itaandaa uchaguzi wa viongozi wake kesho Juni 29, katika mkahawa wa uwanja wa Kasarani.
Wanachama 2,706 waliojisajili kuwa wapiga kura wataamua hatima ya uongozi wa klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Uchaguzi huo unaonndaliwa na tume huru ya mipaka na uchaguzi nchini IEBC, umewavutia wagombeaji wanane wa viti vya Mwenyekiti,Katibu Mkuu na Mtunza Hazina.
Vincent Enos Mutoka, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa zamani wa mauzo katika timu hiyo kutoka tawi la Legends anawania Uenyekiti dhidi ya Mchezaji wa zamani wa timu hiyo Boniface Ambani wa tawi la Diaspora.
Kiti cha Katibu Mkuu kinawaniwa na Irene Wekesa,Isaac Mulanda na Robert Khamala, wakati wadhfa wa mtunza hazina ukiwavutia waaniaji watatu;Edwin Chamwada,Patrick Kanyangi na Newton Luchacha.
Mwenyekiti mpya atakayechaguliwa atamrithi mechezaji wa zamani wa klabu hiyo Dkt.Dan Shikanda ambaye amehudumu kwa kipindi cha miaka miaka minane.