Naibu Rais Rigathi Gachagua alikuwa miongoni mwa mamia ya viongozi wa dunia waliokusanyika mjini Pretoria kuhudhuria hafla kuapishwa kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Ramaphosa alichaguliwa tena kuwa Rais wa nchi hiyo kwa muhula wa pili kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo Mei 29, 2024. Kisha alichaguliwa na wakati wa kikao cha kwanza cha bunge la nchi hiyo kuendelea kuhudumu katika wadhifa huo.
Gachagua alimwakilisha Rais William Ruto kwenye hafla hiyo ya kufana iliyoandaliwa katika majengo ya Union Buildings mjini Pretoria na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na serikali pamoja na Marais wa zamani kutoka ndani na nje ya Afrika.
Wakati wa hafla hiyo, Naibu Rais aliwasilisha ujumbe wa pongezi na kila la heri wa Rais Ruto kwa Rais Ramaphosa na watu wa Afrika Kusini.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga pia alihudhuria hafla hiyo iliyoshuhudiwa na malefu ya raia wa Afrika Kusini.
Raila anamezea mate wadhifa wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Gachagua aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa O.R Tambo mjini Johannesberg muda mfupi baada ya usiku wa manane jana Jumatano usiku.
Aliandamana na Maseneta Lenku Seki wa Kajiando na Karungo Thang’wa wa Kiambu.
Wote hao walilakiwa na Balozi wa Kenya nchini Afrika Kusini Jane Ndurumo.