FKF kumchunguza Matasi, kashfa ya kupanga matokeo

Fadhili Athumani
3 Min Read
Patrick Matasi

Siku ya Alhamisi Machi 27, 2025,  anga ya michezo hapa nchini ilikumbwa na wingu zito la madai ya kuhusika kwa Kipa wa zamani wa timu ya taifa, Harambee Stars, Patrick Matasi katika kashfa ya upangaji wa matokeo.

Kupitia kwa video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Matasi ambaye anachezea klabu ya Kakamega Homeboyz inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini (KPL), alionekana akizungumza na watu wanaodaiwa kuwa ni ‘mawakala’ katika harakati inayodaiwa ya kupanga matokeo ya mechi za ligi kuu.

“Narudia tena mbele ya bosi, hii ni biashara ya kwanza, nakuomba sana,” ilisikika sauti ya mtu asiyejulikana huku Matasi akionekana akitingisha kichwa kukubaliana na aliyoelezwa. Mtu huyo akaongeza, “Unajua jinsi tunavyofanya haya mambo, sijawahi kukuangusha, na wewe hujawahi niangusha.” hii ikimaanisha kuwa wawili hao ni watu wanaojuana.

“Katika biashara zetu huwa hakuna kufeli si ni kweli? Mtu huyo aliuuliza na Matasi akasema ni kweli. Hata katika mkanda huo uliozua gumzo mtandaoni, haijulikani ni ratiba gani waliyopanga kupanga matokeo yake, wala ni lini na wapi iliporekodiwa.

“Chochote nitakacholipwa, nitakutumia moja kwa moja bila kuficha. Baada ya kukutumia nitakupatia simu uongee na ‘bosi’ uthibitishe kupokea mzigo, na mara moja kazi ifanyike,” mtu huyo ambaye mpaka sasa hajajulikana alisikika akimwambia Matasi ambaye aliendelea kukubaliana naye.

Mazungumzo hayo yanaendelea ambapo mtu huyo anayetoa maelekezo anasikika akimwelekeza Matasi jinsi upangaji wa matokeo ya mechi hiyo isiyojulikana itakavyofanyika, “Hii biashara nataka ifanyike katika kipindi cha kwanza, halafu sitaki watu wajue.”

Kwa upande wake, Shirikisho la soka nchini (FKF), limeanzisha uchunguzi juu ya kashfa zinazomkabili Patrick Matasi ambaye katika kipindi ambacho amekuwa langoni Harambee Stars, amekuwa akituhumiwa kujifungisha kizembe hususani katika mechi ambazo Stars ingestahili ushindi.

FKF ya sasa ya Hussein Muhammed na MacDonald Mariga, iliyoingia madarakani hivi karibuni, imewahakikishia wadau na mashabiki wa soka nchini, kufanya uchunguzi wa kina na kwamba ripoti ya uchunguzi huo itafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za soka na katiba ya Kenya.

“FKF inachukulia swala la uadilifu michezo kwa uzito mkubwa. Uchunguzi umeanza na tuwahakikishie tu kuwa, sheria itafuatwa na adhabu stahili itatolewa kwa wote watakaopatwa na hatia. Tutashirikiana na vyombovya usalama kuhakikisha swala hili linashughulikiwa”, ilisema taarifa ya FKF.

Fadhili Athumani
+ posts
Share This Article