Tumbuizo la mwanamuziki Kendrick Lamar wakati wa mapumziko kwenye kinyang’anyiro cha Super Bowl lilivutia lalama kutoka kwa watazamaji kadhaa ambao waliwasilisha malalamishi hayo kwa FCC.
Federal Communications Commission – FCC ni tume huru nchini Marekani ambayo inasimamia mawasiliano ya umma kupitia vifaa kama redio, runinga na hata satelaiti.
Baadhi ya malalamishi ni kuhusu maneno yasiyofaa ya nyimbo, mitindo mibaya ya densi na mandhari yaliyoonekana kuwa kinyume na Marekani.
Kulingana na jumla ya malalamishi 125 yaliyowasilishwa, onyesho hilo la Februari 9, 2025 halikuwa faafu kwa utazamaji wa familia.
Kendrick amelaumiwa kwa kutumia maneno machafu, kutumia watumbuizaji weusi pekee na kuonekana kusababisha mgawanyiko maksudi jukwaani.
Wengine walilalamikia hatua yake ya kushika sehemu zake za siri mara kadhaa jukwaani huku wengine wakilalamika kwamba alitumia tumbuizo hilo kama jukwaa la kumtupia maneno adui yake Drake.
Lamar anaripotiwa kumnyoshea Drake kidole cha lawama kwa kile alichokitaja kuwa mtu anayedhulumu watoto kingono wakati aliimba mtindo wake wa wimbo “Not Like Us”.
Serena Williams naye ametajwa katika baadhi ya malalamishi huku akilaumiwa kwa kushabikia hulka ya watu kuhusika kwenye magenge huku Kanye West akilaumiwa kwa tangazo la kibiashara.
Onyesho la Kendrick Lamar kwenye Super Bowl hata hivyo lilitizamwa na watu milioni 133.5 na huenda ikawa malalamishi ya watu 125 pekee hayatambabaisha.