Bingwa mara mbili wa Olimpiki na dunia katika mbio za mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon atashuka katika uwanja wa kitaifa wa Budapest Jumanne usiku akilenga kuandikisha historia kuwa mwanamke wa kwanza kushinda mataji matatu ya dunia mtawalia.
Kipyegon aliye na umri wa miaka 29 atatimka fainali hiyo kuanzia saa nne na dakika 31 usiku akishirikiana na mwenzake Nelly Chepchirchir.
Kipyegon atashiriki fainali ya Jumanne akiwa roho juu baada ya kusajili matokeo bora msimu huu ikiwemo kuvunja rekodi tatu za dunia mwaka huu ya mita 1,500, ya mita 5,000 na maili moja.
Mwanariadha huyo alishinda dhahabu ya kwanza ya dunia katika shindano hilo mwaka 2017 kabla ya kunyakua shaba mwaka 2019 na kutwaa ubingwa mwaka jana mjini Oregon nchini Marekani.
Fainali ya pili itakayowashirikisha Wakenya ni mita 3,000 kuruka viunzi na maji kuanzia saa nne na dakika 42.
Simon Kiprop, Leornard Bett na Abraham Kibiwott watatimka fainali hiyo wakimenyana dhidi ya bingwa mtetezi Soufiane El Bakkalli wa Morocco.
Kenye ilipoteza taji hiyo kwa mara ya kwanza mwaka jana baada ya kutawala kuanzia mwaka 2007.
Mashindano mengine ya Wakenya leo Jumanne ni raundi ya kwanza ya mita 800 wanaume ikiwashirikisha bingwa mtetezi Emmanuel Korir akishirikiana na Ferguson Rotich, Alex Kipngetich na Emmanuel Wanyonyi kuanzia saa mbili na dakika 20 usiku.
Hadi sasa, Kenya imejishindia nishani moja ya fedha kupitia kwa Daniel Simiu Ebenyo.