Mahakama Kuu mjini Murang’a imempata Ezekiel Saitabu Nakola na hatia ya kuua mama ya mhubiri maarufu Pius Muiru, Grace Wangari Mwangi Machi 20, 2017.
Nakola alikuwa ameajiriwa kama mfanyakazi wa shambani nyumbani kwa mama huyo, katika eneo la Karega, kaunti ndogo ya Kigumo.
Katika uamuzi wake jana Jumatano, Jaji Kanyi Kimondo alisema kwamba ushahidi uliowasilishwa mahakamani unathibitisha kwamba Nakola alitekeleza uhalifu huo.
“Hata ingawa hakuna walioshuhudia utekelezaji wa uhalifu huo au mtu aliyekiri, mazingira ya kesi hii yanaashiria kwamba mshtakiwa ana hatia,” ilisema taarifa ya afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP.
Nakola anasemekana kumtoa uhai mama Grace kwa kumyonga kabla ya kuzika mwili wake nyuma ya zizi la ng’ombe na kufunika kaburi hilo na mchanga na migomba ya ndizi kabla ya kuiba pesa kutoka kwenye simu yake ya rununu.
Eneo hilo lilikuwa limetumiwa awali kuzika mzoga wa ng’ombe.
Alikuwa amefanya kazi kwenye boma la mama Grace kwa miaka 10 kabla ya kutekeleza uhalifu huo.
Atahukumiwa Septemba 19, 2024.