Edgar Lungu azuiwa kufanya mazoezi hadharani

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, ameonywa dhidi ya matukio yake ya kukimbia hadharani, huku polisi wakielezea mazoezi yake kama “harakati za kisiasa”.

Katika taarifa yake polisi ilisema vikao vya mazoezi vya Bw Lungu huku akisindikizwa na wanachama wa chama chake cha Patriotic Front (PF) na bila maafisa wake wa usalama vimefikia kiwango cha kuwa “kusanyiko lisilo halali”.

Mkuu huyo wa zamani wa nchi aliamriwa kuwaarifu polisi mapema wakati wa kupanga mazoezi yake katika siku zijazo “kuhakikisha usalama wa umma na usimamizi wa trafiki”.

“Bw Lungu anapaswa kuzingatia kikamilifu itifaki za usalama na ajiepushe na aina yoyote ya harakati za kisiasa,” msemaji wa polisi Rae Hamoonga alisema.

Haya yanajiri siku chache baada ya Bw Lungu kupeleka serikali mahakamani baada ya kudaiwa kumzuia kusafiri kwenda Korea Kusini kwa mkutano. Baadaye aliondoa kesi hiyo mahakamani.

Baada ya kuwa mamlakani kwa miaka sita Bw Lungu alishindwa katika uchaguzi wa urais wa 2021 na Hakainde Hichilema.

Anaaminiwa kuwa anapanga kurejea katika uchaguzi wa 2026.

Share This Article