Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC imetoa mwaliko kwa mbunge wa Kimilili Didmus Barasa afike mbele yake kesho Jumanne Agosti 27, 2024 kujibu madai ya utapeli.
Barasa anadaiwa kutapeli mama mmoja mfanyibiashara shilingi milioni 2 kwa ahadi kwamba angemsaidia kupata zabuni za serikali.
EACC inasema kwamba baada ya kupokea pesa hizo, Barasa alikatiza mawasiliano na mfanyibiashara huyo tangu Disemba mwaka jana huku akizuia njia zote za mwanamke huyo kumfikia.
Tume hiyo inasema pia kwamba Barasa alikosa kutii mwaliko wa awali kuhusu kesi hiyo hiyo Agosti 14, 2024 na sasa imempa fursa nyingine kesho saa tatu asubuhi.
Onyo limetolewa kwa mbunge huyo kwamba iwapo atakosa kufika mbele ya EACC tena, kesi hiyo itakamilishwa na maamuzi kufanywa bila yake kuwepo.
Inaripotiwa kwamba Barasa alitumia wadhifa wake bungeni wa mwenyekiti wa kamati ya barabara kumshawishi mwanamke huyo kumpa shilingi milioni mbili ili amsaidie kupata zabuni za kutengeneza barabara.
Milioni hizo mbili aliambia mfanyibiashara huyo kwamba ni dhihirisho la kujitolea kwake kupata zabuni hizo.
Disemba 13, 2023 mwanamke huyo aliweka pesa hizo kwenye akaunti ya benki ya Barasa ambaye baada ya kuzipokea alikatiza mawasiliano naye.
Barasa amekanusha madai ya kumtapeli mama huyo akisema kwamba alimpa pesa hizo kama mkopo.