Tume ya Maadili na kukabiliana na ufisadi, EACC, imefichua kwamba fedha kutoka kwa hazina ya Inua Jamii, hutumwa kwa watu waliostaafu na waliofariki, huku wanaolengwa na hazina hiyo wakiendelea kukumbwa na masaibu.
Ikiwasilisha ripoti yake kwa idara ya utunzi wa jamii, tume hiyo ilidokeza kuwa hazina hiyo haina mfumo mwafaka wa kuwatambua wanaostahili kunufaika na fedha hizo.
“Miongoni mwa maswala yaliyogunduliwa ni hatua ya kutuma pesa kutoka hazina hiyo kwa watu waliofariki na wanaonufaika na malipo ya kustaafu, huku wanaopaswa kunufaika na hazina hiyo wakiachwa bila mapato,” ilisema taarifa hiyo.
Kulingana na tume hiyo, uchunguzi huo uliofanywa kati ya Aprili 5, na Mei 22, 2024, ulilenga kutambua na kuziba mianya, ambayo huenda inatumiwa kuiba pesa za umma kupitia hazina hiyo.
Katibu wa idara ya serikali ya utunzi wa jamii Joseph Motari, alipokea ripoti hiyo iliyowasilishwa kwake na kamishna wa EACC Alfred Mshimba.
Rais William Ruto aliagiza pesa za hazina hiyo ziwe zikitolewa kufikia tarehe 15 kila mwezi.