Beatrice Chebet ametetea taji ya dunia ya kilomita 10 katika makala ya 45 ya mashindano ya mbio za nyika Jumamosi alasiri mjini Belgrade nchini Serbia.
Chebet aliyekuwa akitetea taji ya mwaka 2023, alitoka katika nafasi ya tano na kukata utepe wa kwanza kwa dakika 31 na sekunde 5 huku fedha ikitwaliwa na Lillian Kassait kwa muda wa dakika 31 na sekunde 8 wakati Margaret Chelimo akijizolea shaba kwa dakika 31 na sekunde 9.
Wakenya walinyakua nafasi tano za kwanza katika shindano hilo.
Kenya pia ilinyakua dhahabu na shaba ya kilomita 8 wavulana wasiozidi umri wa miaka 20, Samuel Kibathi akitwaa ubingwa kwa dakika 22 na sekunde 40akif uatwa na Megzebu Sime wa Ethiopia aliyeshinda fedha huku Mathew Kipruto akishinda shaba.
Kenya pia walidhihirisha ubabe katika mbio mseto za kupokezana kijiti kupitia kwa Reynold Kipkorir, Virginia Nyambura, Kyumbe Munguti na Purity CHepkurui.
Hata hivyo, Wakenya waliishia kunawa katika mbio za wasichana chini ya umri wa miaka 20 kilomita 6, Sheilla Jebet akimaliza wa nne huku Ethiopia ikishinda dhahabu, fedha na shaba.