Waziri wa Afya Aden Duale,ametoa onyo kali kwa mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali ya Mediheal Dkt. Swarup Mishra, kuhusu ukiukaji wa maadili za sekta ya Afya.
Waziri huyo alisema Dkt. Mishra huenda akafunguliwa mashtaka, kufurushwa hapa nchini na kufutiliwa kwa uraia wake wa hapa nchini chini ya sheria za uhamiaji, huku ikisubiriwa kupitishwa kwa ripoti ya kamati ya uchunguzi.
Duale aliyasema hayo leo Ijumaa wakati wa kufungwa kwa makala ya 15 ya mashindano ya michezo ya Taasisi za Mafunzo ya Utabibu Nchini (KMTC) katika shule ya upili ya wavulana ya Chebisaas , kaunti ya Uasin Gishu.
Kwenye hotuba yake, waziri huyo alihakikisha kujitolea kwa wizara ya Afya katika kuimarisha nguvukazi kwenye sekta ya Afya.
Alitoa wito kwa KMTC kuendelea kuwekeza kwa michezo, ukuzaji talanta na kuimarisha ushirikiano wa sekta mbali mbali ili kupiga jeki afya ya kiakili, kimwili na kijamii wa wataalam wa Afya.