Waziri wa Afya Aden Duale ametangaza kwamba uchunguzi wa hali ya juu unaendelea katika sekta ya afya kwa nia ya kutambua mianya ya ulaghai na kuchukua hatua.
Duale alifichua kwamba zaidi ya vituo 1,000 vya afya hasa vya kibinafsi vimefungwa na vingine zaidi vinachunguzwa kwa kujaribu kudai fedha kinyume cha sheria kutoka kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA.
Katika hotuba kali siku ya Jumamosi, Duale alitaja kaunti tano kama maeneo hatarishi ya ulaghai huo ambazo ni Homa Bay, Bungoma, Mandera, Wajir na Kisii.
Amesema kuwa vituo vya kibinafsi katika maeneo haya ndivyo vinavyoongoza kwa sifa mbaya.
Alieleza kuhusu msako mkali unaoendelea, akibainisha kuwa tangu tarehe 30 Machi, vituo kumi na viwili vimefungwa kwa tuhuma za ulaghai.
Vituo ishirini na vinne kwa sasa vinafanyiwa ukaguzi wa kitaalamu na wachunguzi maalum kutoka SHA huku idara ya upelelezi wa jinai ikichunguza jumla ya vituo 250.
Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imepokea faili 30 za kesi na vituo 18 tayari vinakabiliwa na mashtaka mahakamani.
Duale, akisisitiza wajibu wake wa kulinda ahadi ya huduma bora za afya kwa wote, aliapa kuwa hata senti moja ya fedha za umma iliyokusudiwa kuwahudumia wagonjwa haitatumika vibaya.
Alisema wizara yake itafanya kazi bila kuchoka kulinda fedha hizi muhimu.
Waziri huyo aliyasema hayo alipokuwa akiongoza sherehe ya mahafali katika kituo cha Hawa Kosar Islamic Centre katika kaunti ya Garissa.
Alipongeza wasichana 25 waliohitimu na kupokea cheti cha masomo ya Kiislamu cha kiwango cha shule ya upili.