Maafisa wanne wa kaunti ya Taita Taveta watafunguliwa mashtaka ya ufisadi na kujipatia mali ya umma kinyume cha sheria.
Hii ni baada ya mashtaka dhidi yao kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga.
Ingonga aliidhinisha mashtaka dhidi ya wanne hao siku moja baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC kuwakamata maafisa hao waandamizi wa kaunti ya Taita Taveta kwa tuhuma za kufuja shilingi milioni saba mali ya umma.
Maafisa hao ni Thomas Jumwa ambaye ni mshauri wa sasa wa masuala ya kiuchumi wa Gavana wa kaunti hiyo, Liverson Mghendi ambaye ni Katibu wa zamani wa kaunti hiyo na Leonard Langat ambaye ni Afisa Mkuu wa zamani wa Fedha. Wote hao walikamatwa ndani ya kaunti ya Taita Taveta.
Mshukiwa wa nne, Christine Wakera ambaye ni Afisa Mkuu wa zamani wa Biashara, Utalii na Ustawi wa Vyama vya Ushirika alikamatwa mjini Eldoret.
Kwenye taarifa, Msemaji wa EACC Eric Ngumbi aliesema washukiwa hao walikamatwa kwa tuhuma za kufuja shilingi hizo milioni saba kwa kusingizia kuwa wanafanya maadhimisho ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia kati ya Novemba 24 na 27, 2022.