Dorcas Rigathi: Sheria za kukabiliana na mihadarati ni hafifu

Tom Mathinji
1 Min Read

Mke wa naibu Rais mchungaji Dorcas Rigathi, ameelezea wasiwasi wake kwamba sheria za humu nchini haziwachukulii hatua kali walanguzi wa dawa za kulevya, wahusika wakuu kwenye biashara hiyo, pamoja na watengenezaji pombe haramu.

Akizungumza Jumanne wakati wa mkutano wa viongozi wa kidini kwenye kanisa moja eneo la Kabete kaunti ya Kiambu, Dorcas, alisikitika kuwa ” sheria ni hafifu kwa wauaji wa watoto wetu,”.

Aidha aliapa kukabiliana vilivyo na uraibu wa dawa za kulevya na unywaji pombe, kupitia kampeini aliyoanzisha mwaka uliopita.

“Ikiwa sheria haitakabiliana na uraibu huo, tutapigana vita dhidi ya mihadarati kupitia nguvu za kiroho. Lazima tuwapatie tumaini, nguvu na tuwatie motisha,” alisema Dorcas.

Alitoa changamoto kwa kanisa kuzungumzia swala hilo kwa minajili ya ustawi wa Wa-Kenya, hasa vijana.

Kwa upande wake naibu gavana wa kaunti ya Kiambu Rosemary Kirika, aliwaonya wakazi wa eneo hilo dhidi ya utumizi wa pombe kutokana na madhara yake katika mwili wa binadamu

Share This Article