Mkewe Naibu wa Rais Dorcas Rigathi ameelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya tumbaku katika kaunti ya Laikipia.
Akiongea alipozindua kambi ya siku mbili ya matibabu katika uwanja wa Rumuruti, Dorcas alisema kuwa watumizi wengi wa tumbaku wanakabiliwa na hatari ya kuathiriwa na maradhi ya akili, pamoja na maradhi mengine yanayotokana na bidhaa hiyo.
Alisema kuna haja ya kubadilisha mkondo huo ili kuzuia kupoteza watu wengi kwa uraibu huo wa tumbaku.
Kulingana naye, asilimia moja ya wanawake nchini hutumia tumbaku huku kaunti ya Laikipia ikiwa na asilimia mbili ya watumizi.
Asilimia 13 ya wanaume nchini Kenya hutumia tumbaku huku idadi ya watumizi huko Laikipia ikiwa asilimia 17.
“Nchini Kenya, asilimia moja ya wanawake hutumia tumbaku, hapa Laikipia asilimia mbili ya wanawake wanatumia tumbaku. Kwa upande wa wanaume, asilimia 13 hutumia tumbaku hapa Kenya, hapa Laikipia asilimia 17 wanatumia tumbaku. Kutokana na hayo, tumeanza kuwapoteza wanawake na wanaume kwa ugonjwa wa saratani, na tunaomba kuwe na mabadiliko ili tusiwapoteze watu,” alisihi Dorcas.
Kambi hiyo ya siku mbili ya matibabu bila malipo, inalenga mtoto wa kiume aliyeathiriwa na uraibu wa pombe na mihadarati na jamii yote kwa ujumla.
Mkewe Naibu wa Rais pia alielezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa visa vya mimba miongoni mwa wasichana wadogo katika kaunti ya Laikipia.
“Takriban asilimia tisa ya wasichana walio na umri wa kati ya miaka 15-19 wamekumbwa na visa vya mimba za mapema, na takwimu zinaashiria kwamba tunapaswa kushughulikia swala hili mapema,” alisema Dorcas.