Abiria 33 walipata majeraha baada ya basi walimokuwa wakisafiria, kuhusika katika ajali ya barabarani katika kituo cha kibiashara cha Tunnel, kaunti ndogo ya Kipkelion Magharibi.
Basi hilo lilikosa mwelekeo katika barabara ya Forte Tenan – Muhoroni , na kuangaka ndani ya mtaro.
Akithibitisha ajali hiyo iliyotokea Alhamisi, kamanda wa polisi wa kaunti ya Kericho Geoffrey Mayek, alisema dereva wa basi hilo alipoteza mwelekeo alipojaribu kuepuka kugonga lori lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara.
Abiria hao waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali ya Forte Tenan na ile ya rufaa ya kaunti ya Kericho kwa matibabu.
Kulingana na Mayek, basi hilo lilikuwa likielekea Busia wakati ajali hiyo ilipotokea, huku akithibitisha kuwa hakukuwa na maafa.
Alitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za trafiki na kuwa waangalifu hasaa wakati huu wa msimu wa krismasi.