Huku awamu ya pili ya utoaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio ikianza siku ya Jumapili, wizara ya afya imesisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama kwa watoto.
Mkurugenzi Mkuu wa afya Dkt. Patrick Amoth, ameondoa hofu kwamba vifo vya watoto wawili vilivyoshuhudiwa wakati wa utoaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio kati ya tarehe 2 na 6 mwezi Oktoba, vilitokana na chanjo hiyo.
Dkt Amoth alihakikishia umma kuhusu usalama wa chanjo hiyo, akisema vifo vya watoto hao na athari hizo mbaya vilitokana na sababu zingine wakati wa chanjo hiyo.
“Wizara ya afya inahakikisha kuwa chanjo zote,zikiwemo za polio ni salama, na zinawakinga watoto dhidi ya maambukizi ya mahonjwa yanayoweza epukika,” alisema Dkt. Amoth.
Amoth aliwahakikishia wazazi kwamba watoto wao wako salama, akiwahimiza waendelee kuchanja watoto wao na kushiriki katika awamu ya pili ya siku tano ya chanjo ya polio ambayo ilianza jana Jumapili na inatarajiwa kukamilika Jumatano tarehe 13 mwezi Novemba mwaka 2024.
Haya yanajiri baada ya chanjo ya hivi majuzi iliyotolewa kati ya tarehe 2 na 6 mwezi Oktoba, kudaiwa kusababisha vifo vya watoto wawili kati ya milioni tatu waliolengwa kwa chanjo hiyo, na kuibua wasiwasi wa kiafya kuhusu usalama wa chanjo za polio