Diamond ampa Mzee Makosa milioni 10

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz ambaye jina lake halisi ni Naseeb Abdul leo amekutana na Mzee Makosa na kumtunukia zawadi ya shilingi milioni 10, pesa za Tanzania.

Diamond ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Wasafi Media aliguswa na simulizi ya maisha ya Mzee Makosa aliyehojiwa na Wasafi Media katika kipindi cha yaliyovuma almaarufu “Yaliyo-Trend”.

Makosa ambaye jina lake halisi ni Ramadhani Mrisho Kasawa alisimulia jinsi alifilisika licha ya kuwa na utajiri wa kiwango cha juu awali.

Mzaliwa huyo wa mkoa wa Iringa alisema kwamba hata ingawa hakusoma sana, alikuwa na ari ya kusafiri nje ya Tanzania akiwa kijana.

Alifanikiwa kusafiri hadi Ulaya ambako alipata ajira kwenye meli kama mtu wa kupakulia wahudumu wa meli chakula, kazi iliyomfanya asafiri sehemu mbali mbali.

Pesa alizopata anasema aliweka akiba katika benki nchini Italia kwa miaka 10 baada ya hapo akarejea Tanzania mwisho wa mwaka 1993.

Biashara ya kwanza aliyoingilia ni ya usafirishaji wa watu na bidhaa kupitia basi dogo aliloagiza kutoka Japan. Anasema alikuwa anafanya kazi hiyo mchana na usiku.

Nyingine aliyoingilia baada ya kupata mapato kutokana na usafirishaji ni hospitali ya kibinafsi. Baadaye aliongeza magari ya uchukuzi na hata kujinunulia gari la kutembelea binafsi.

Alifungua pia sehemu ya burudani ambayo ilikuwa hata na vyumba vya kulala, biashara ambayo anasema aliingilia kwa sababu ya kupenda muziki na wanawake.

Kulingana naye, umaskini ulianza kuingia mwaka 2011, pale ambapo waliokuwa wakimfanyia kazi walianza kumwibia huku akipoteza mali zake kwa njia ya utata.

Alimshukuru Diamond kwa usaidizi wa kifedha aliompa.

Share This Article